Sports and Entertainment

Jumanne, 15 Julai 2014

Mkuu wa mkoa apewa wiki afute kauli yake "bodaboda" kuingia mjini

Hakuna maoni :

Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki.
Kamati ya Madereva wa Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam wameipa siku saba serikali ya mkoa huo kufuta agizo la kuzuia pikipiki, maarufu kama ‘bodaboda’ kufanya shughuli zake katikati ya jiji, vinginevyo, wataitisha maandamano ya amani pamoja na kwenda mahakamani kudai haki yao.

Imesema wamebaini kuwa zuio hilo lilitolewa Machi 3, mwaka huu na Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, bila uhalali, ikiwa ni pamoja na kutotambuliwa na sheria na kutokuwapo kwenye maandishi yanayotumiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini nchini (Sumatra).

Katibu wa Kamati hiyo, Daudi Laurian, alisema agizo hilo limelenga kuwanyima ajira vijana, haki na linavunja sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 13, pamoja na ile ya leseni za usafirishaji iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009.

“Katika uchunguzi uliofanywa na kamati, tumegundua kuna ubaguzi, ambao unafanywa, kwani kuna bodaboda, ambazo bado zinafanya kazi hiyo katikati ya mji.

Pia zuio hili halina uhalali wowote na hakukuwa na taarifa iliyo katika maandishi kwenda katika vyama vya waendesha bodaboda wilaya za Temeke, Kinondoni na Ilala na kwa wadau wengine,” alisema Laurian.

Alisema madai ya mkuu wa mkoa kwamba, bodaboda zinasababisha ujambazi hayana ukweli, kwani yamelenga kujenga utetezi wa kushindwa kuwajibika kwa vyombo vya usalama pamoja na kushindwa kuonyesha mipaka ya mjini kati kwa ufasaha.

“Kama kweli bodaboda tunasababisha ujambazi na uhalifu mwingine, mbona serikali isizuie uuzwaji wake? Pia hatukupewa hata notisi ya kwenda kwa wadau. Pia jiji wanatumia sheria zipi? Za kibaguzi za kutoa vibali vya kibaguzi kwa pikipiki kuingia mjini kati?” alihoji Laurian.

Alisema baada ya agizo la zuio la bodaboda kutolewa wamekuwa wakiishi kwa hofu, kwani huvamiwa na majambazi, ikiwamo kutoa mwanya kwa taasisi za usalama na watu binafsi kutekeleza kuwakamata madereva na kuwatoza faini, kuanzia Sh. 50,000 hadi 450, 000.

Hata hivyo alisema kamati ikiwa inaendelea na mazungumzo ya kutatua mgogoro huo kati yao na ofisi ya mkuu wa mkoa, jiji, Sumatra, manispaa wanataka madereva waliopo mahabusu wachiwe huru pamoja na kuwaruhusu kuingia mjini kwa kuwatengea vituo maalumu vinavyotambulika kisheria.


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni