Ijumaa, 25 Julai 2014
BARUA YA WAZI KWA DIAMOND PLATNUMZ
Nasibu Abdul ‘Diamond’. Bila shaka utakuwa mzima wa afya njema mdogo wangu. Mimi nipo poa, naendelea na mchakamchaka wa maisha kama kawaida. Leo nimekukumbuka kwa barua.Nikuambie ukweli, barua hii naandika kwa hisia kali sana, nikiwa na lengo la kukushauri jambo jema ambalo litayafanya maisha yako yaendelee kuwa mazuri bila vikwazo.
Kuna kitu kinaendelea ambacho ukikitazama kwa juujuu unaweza kuona ni kidogo lakini ukitafakari kwa kina utaona namna lilivyo na umuhimu mkubwa katika maisha yako.Ni kuhusu baba yako mzazi, mzee Abdul Jumaa. Sitaki kuingilia maisha yako, si lengo langu kukupangia namna ya kuishi lakini nalazimika kukushauri kwa upendo kabisa, ushauri ambao una uhuru wa kuupokea au kuuacha.
Nimefanya hivyo mara nyingi kwako kuhusiana na mambo mbalimbali, ndani na nje ya muziki wako wa Bongo Fleva. Nakuomba utulize moyo.Usishangazwe na namna mambo yako binafsi ya kifamilia yanavyoingiliwa kwa sasa. Hiyo ni kwa sababu ya ustaa wako. Wewe ni mtu wa jamii.
Watu wanajitazama kupitia kwako.Inaelezwa kuwa baba yako kwa sasa ni mgonjwa na hana msaada wa matibabu. Maelezo yanasema kuwa, kwa muda mrefu huna maelewano na mzazi wako huyo.
Sitaki kuingia ndani sana, wala sihitaji kujua sababu ya kutokuwa na maelewano na mzazi wako lakini kwa uchunguzi niliofanya, inaonyesha kuwa, mzee wako anakupenda kama mwanaye na yupo tayari kushirikiana na wewe.
Kuna wakati nilimsikia mzee akisema, hahitaji fedha zako (akimaanisha si kwamba anataka kuchukua utajiri wako) bali anatamani uhusiano wako na yeye, kama mtu na baba yake urudi!Hiyo ni busara ya hali ya juu. Diamond nataka kukuambia jambo moja mdogo wangu, zipo baraka nyingi sana kupitia kwa wazazi.
Kwa bahati mbaya, wazee wamepewa nguvu ya kuamua maisha ya watoto wao.Mzazi akikasirika anaweza kutamka neno baya likakufika. Amini usiamini, ipo hivyo na haiwezi kubadilika.
Hata vitabu vitakatifu vinaeleza hivyo waziwazi.Kuna mahali kwenye maandiko kumeandikwa: Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako.Andiko hilo pekee linatosha kutuongoza kuwaheshimu wazazi kwa kila namna.
Inawezekana kuna mambo ambayo mzee wako ameyafanya yakawa kikwazo kwako, isiwe tabu. Waswahili wanasema: Mkubwa hakosei, anasahau tu!Chondechonde mdogo wangu, rudisha uhusiano mwema na mzazi wako, baraka zitazidi na Mungu atakuongezea katika shughuli za mikono yako. Nitafurahi kama utaelewa na kuyafanyia kazi.Yuleyule,
Mkweli daima,
Mkweli daima,
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni