Sports and Entertainment

Jumanne, 22 Julai 2014

kuhusu semina iliyoendeshwa na David Banner, Terrence J, Chaka Zulu na Ravi Shelton

Hakuna maoni :

Jifunze yaliyojiri katika semina iliyoendeshwa na David Banner, Terrence J, Chaka Zulu na Ravi Shelton


    July 14, 2014 wasanii na wadau mbalimbali wa sanaa ya muziki na filamu Tanzania waljumuika katika ukumbi wa Bank Kuu ya Taifa (BOT) kuhudhuria seminar kwa lengo la kupata elimu na kushare uzoefu wa biashara ya filamu na muziki kutoka Marekani.
    Semina hiyo iliendeshwa na wamarekani David Banner (rapper, producer aliyefanya kazi na wasanii wakubwa Marekani na mshindi wa tuzo ya Grammy), Chaka Zulu( Meneja wa wasanii na mwanzilishi wa wa label ya DTP ), Terrence J (Muigizaji, mtangazaji wa TV na mwandishi wa vitabu) na Ravi Shelton ambaye ni mfanyabiashara na mtaalamu wa masuala ya endorsement za wasanii.
    Binafsi nilifika katika jengo ukumbi wa BOT mida ya saa nne na nusu na kuanza kuyazoea mazingira mapema huku macho yangu yakihesabu bila kutaja namba wasanii wakubwa, mameneja, watu wa media na wadau wakubwa wa tasnia ya muziki na filamu kwa ujumla Tanzania, na  kwa haraka haraka ukumbini tulikuwa kati ya watu 200 na mia tatu kasoro.
    Mbele ya umati huo kulikuwa na meza kubwa  ambayo walikaa waongozaji kutoka Tanzania waliojitambulisha kwa majina na vyeo. Alikuwepo Addo November, rais wa shirikisho la muziki Tanzania, Dr Mona toka chuo kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha sanaa, Seven Mosha ambaye ni muwakilishi wa kampuni ya Sony Music Entertainment.
    Kabla semina halisi haijaanza na wageni hawajaingia ukumbini, wahudhuriaji walitahadhalishwa kuwa wasijikite katika kueleza matatizo ya kiwanda cha sanaa Tanzania kwa kuwa jamaa wamekuja kufundisha na kushare walichonacho sio kupokea kero na kuzifanyia kazi.
    Kwa hiyo ikatolewa saa moja na nusu hivi kila mtu kutoa sumu ya alichonacho kabla kupitia mdahalo usio rasmi na hapo likapigwa zogo kali. Kikubwa kikiwa ni wasanii kunyonywa na mfumo, kutokopesheka na mabenki, kutopata sapoti kutoka COSOTA ambapo palirushiwa lawama nyingi zaidi kuwa sehemu kubwa ya wafanyakazi wake wamelala. Pia changamoto ya utaratibu wa stika za TRA. Vilio vya njia za uuzwaji wa CD, Miito ya simu n.k. Kila mtu alisema yake ambayo wengi tumeyazoea huku vitendo dhidi yake vichechemea.
    Hata hivyo, zogo hilo lilionekana kukorea na watu kushambulia zaidi huku lawama nyingine zikielekezwa kwao kuwa wengi wao hawafuati utaratibu japo wanalia, wengi hawajajiandikisha COSOTA na hata hawana TIN number ya TRA kwa biashara ya muziki wanayofanya.
    “Wasanii wa Tanzania wanaweka nguvu nyingi sana kwenye sanaa na sio kwenye biashara.” Alisema Seven Mosha, point ambayo ilikubaliwa na wengi kama kilio kipya kwa wengi cha ushuru mkubwa wa vifaa vya muziki vinavyoingia nchini.
    Kama unavyoelewa watanzania tuna mengi yakusema tukipewa nafasi, zogo liliendelea huku point za msingi zikimiminika hadi walipoingia waendesha seminar waalikwa. Hapo mic ya Mkubwa Said Fella ilikuwa ON na zamu yake lakini kwa busara aliamua kuahirisha alichotaka kusema ili shule ianze rasmi.
    Baada ya utambulisho wa majina na mada, liliibuka suala la hofu ya uelewa wa lugha kati ya baadhi ya wahudhuriaji na ukizingatia yai lililokuwa linavunjwa ni la kwao ‘2Chainz na Jay Z’ sio yai la kinaija! LOL.
    Hata hivyo, ombi la kuwepo mtafsiri lililotolewa liligonga ukuta baada ya kugundua kuwa muda usingetosha. Kwa hiyo ukweli ni ukabaki kuwa kuna baadhi ya wajumbe walitoka patupu licha ya kuwepo hadi mwisho.
    By the way, kuna walichopata kama  zogo la kibongo na picha za instagram..LOL!
    Bila kupoteza muda, shule ilianza na mimi nikajikunja na ‘kinotibuku’ changu na kalamu kuhakikisha naandika vyema kinachoelezwa, kwa faida yangu na kuhakikisha napata vyema cha kuiambia Tanzania kupitia The Jump Off  ya 1005 Times Fm na kupitia kalamu hii.
    Mada ya kwanza ilihusu namna msanii anavyoweza kujiendeleza kama bidhaa ikiwa na vipengele vilivyomeza  mfumo wa biashara ya sanaa, mfumo wa menejimenti ya msanii, fursa zinazokuja, mipango ya kujiendeleza na mengine mengi. Sitaki turudi darasani kiivo, ngoja nikugusie kile walichosema wanyamwezi.
    Chaka Zulu alianza kueleza jinsi msanii anavyotengenezwa kwa kueleza kuwa mfumo wanaoueleza ni wa Marekani lakini wanaamini kupitia huo watanzania wanaweza kuja na mfumo wao ambao unaweza kuwa bora zaidi.
    Kwa ufupi, msanii alichukuliwa kama bidhaa ambayo ina kitu kinachohitajika sokoni lakini kuna mnyororo ambao inabidi utengenezwe ili bidhaa itengenezwe vyema na iuzike.
     Hapo yakazungumziwa masuala ya kuajiri menejimenti ambayo malipo yake yatatoka kwenye matunda ya  kazi kwa kutaja asilimia ya matunda na sio kiasi cha pesa, hivyo kadri mtakavyovuna ndivyo mtakavyogawana matunda na menejimenti, mwanasheria, producer na wengine kuwa kila mmoja ana nafasi yake kubwa ya kuitengeneza na kuiuza bidhaa (Msanii/alichonacho).
    Somo hilo liligusa sintofahamu ya ugawanaji wa mapato ya kazi ya muziki kati ya msanii, mwandishi na producer kwa Tanzania, ambapo walieleza kuwa kwa Marekani matunda ya kazi hugawanywa kwa asilimia na kila mshiriki anakula chake.
    Walisema kwao, matunda hugawanywa 50% (midundo, melodies na rhythm za vyombo), na 50% (Uandishi, na maneno/sauti). Kwa hiyo hapo mwandishi kama sio muimbaji ana 25% ya matunda ya wimbo. Kama msanii ndiye amefanya vingi zaidi atapata mengi zaidi, lakini kama ameimba tu ina maana ana 25% ya matunda.
    Lakini pia kuna uwanja wa makubaliano kama pande zote mbili zitapanga kufanya makubaliano mengine kwa jinsi walivyofanya kazi.
    Kingine kikubwa kilichogusiwa na wajumbe wakaambiwa kukipigia msitari ni suala la haki miliki ambayo kwa Tanzania ilionekana kama kitendawili. 
    “Haki miliki ni ASSET yako. Kama hauimiliki basi hauna kitu.” Alisema David Banner.
    Mfumo wa kazi na mgawanyo wa matunda unaenda hadi kwa menejimenti na kila mtu anaehusika na project na hapo ndipo msemo wa ‘Utakula Ulichoua’ unaingia. Mgao unategemea kazi ya mtu katika kuuza bidhaa (msanii na kazi yake). Hakuna ushikaji hapo, na kila mtu anapiga kazi ili aendelee kuhitajika zaidi kwenye mradi huo.
    Kipengele kingine kizito kilikuwa msanii/meneja kujitegemea, kutengeneza thamani ndani yake na kuitunza kwa kuwa kuna mtu ataitafuta na kuinunua.
    “Tengeneza thamani ndani yako kwa kuwa na kitu ambacho kupitia hicho msanii/meneja au mteja atamthaminisha na kutaka kufanya biashara kupitia wewe.” Alisema Terrence J.
    Nae David Banner akakazia kuwa kama msanii au meneja hajui thamani yake, kuna mtu atatafuta na kujua thamani yake na atamtumia kutengeneza pesa (bila msanii kufaidika).
    Baada ya mada hiyo ya kwanza ambayo liliambata na kipindi cha maswali na majibu, walizungumzia pia masuala ya soko na jinsi ya kuuza kazi ya sanaa na msanii ambapo kitu cha kwanza kilisisitizwa kuwa ‘kujibrand’ kama msanii na kuwa na utambulisho wa pekee.
    ‘Utambulisho wa pekee’ ulisisitizwa zaidi kuwa licha ya kumsaidia msanii kupenya kwenye soko, utamsaidia kuwepo kwa muda mrefu hata kama akikaa kimya kama ilivyokuwa kwa ‘Nas’, kwa kuwa hakuna copy yake sokoni iliyoweza kumvaa.
    Kingine kwa msanii baada ya kuingia sokoni ni kutambua soko lake ‘target audience’ na kuendana nalo kwa kila kitu hata katika maisha, hii itamsaidia kupata endorsement kwa kuwa watu wanaotaka kupata kundi la watu anaowahudumia wanaweza kupitisha bidhaa zao kwake ili kuwafikia kwa kuwa wako nae.
    Ukatolewa mfano kwa ufafafanuzi. Kama wewe ni msanii wa injili jitahidi maisha yako yaendane na injili ili usiwapoteze watu wako (wasikukute sehemu kama club kwa mfano, kuzingatia aina ya mavazi nk).
    “Find your audience, rock with them and bring them in.” Anakaririwa Chaka Zulu.
    Hata hivyo, kitu kilichowashangaza ni pale walipogundua kuwa hakuna kabisa mfumo rasmi wa uuzaji wa kazi za muziki Tanzania kwa njia ya mitandao wakati kwa upande wao wanategemea sana soko hilo kwa kuuza kupitia iTune, Amazon n.k.
    Walishauri wasanii kutumia vizuri mitandao ya kijamii na kuhakikisha kuwa wanakundi la kutosha la watu kwenye mitandao na kutumia websites pia.
    Walisisitiza kuwa msanii anapaswa kutumia vizuri (effectively and efficiently) idadi yoyote ya mashabiki alionao ambao ni soko lake na kupitia hao wataongezeka.
    Katika pointi ya kujitangaza na kujitanua kimuziki, walisisitiza kuwa wasanii inabidi wapeane sapoti kwanza ya kutosha humu ndani ili wawe wakubwa zaidi na kuongeza nguvu wanapotaka kutoka nje. Sapoti iwe kote hata kwa kufuatana kwenye mitandao ya kijamii na katika njia nyingine. Sapoti ya ndani ilitakiwa kupigiwa mstari kama suala la haki miliki ya kazi za sanaa.
    Yote kwa yote, mengi ya muhimu yalizungumzwa kwenye seminar hiyo na kila mmoja alishika lake, hii ni sehemu tu ya kilichofundishwa.
    Kama umesoma hadi msitari huu naamini umepata picha kidogo ya kile likilichofanyika, endelea kutembelea tovoti ya Times Fm na sikiliza The Jump Off ya 100.5 Times Fm na utawasikia wasanii wakielezea kile walichoondoka nacho.
    Binafsi nilijifunza kitu kwenye hii shule ya bure na kwa kuwa sina kipaji cha  kufundisha nahisi kuna mengi niliyobaki nayo kichwani.
    Lakini swali langu na la wengi, ni kuhusu utekelezwaji wa kilichofundishwa. Je, COSOTA, BASATA, Wasanii, wadau mbalimbali na Serikali kwa ujumla itayafanyia kazi au ni shule tu itakayobaki kichwani baada ya kueleweka?

    Hakuna maoni :

    Chapisha Maoni